Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya Kiislamu ya Al-Wefaq nchini Bahrain imesema kuwa; mwenendo wa utawala unaotawala umeleta pigo kubwa kwa uhuru wa kidini nchini na umeugeuza msimu wa Ashura (maombolezo ya mwezi wa Muharram) kuwa jambo la kiusalama kabisa. Hali hiyo imefichua ukweli nyuma ya madai rasmi ya serikali na kudhihirisha uwepo wa dhulma ya kidini iliyopangwa pamoja na kuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini Bahrain.
Katika taarifa yake yenye anuani "Ashura ya Bahrain Inapaza Sauti: Dhulma, Dhulma", jumuiya hiyo ilieleza kuwa; maadhimisho ya Ashura ya mwaka huu yalifanyika katika mazingira ya juhudi za serikali za kutaka kuyadhibiti maadhimisho hayo kwa mbinu mbalimbali, hali hiyo ilishuhudia kuongezeka kwa wito wa kuwahoji watu, kukamatwa kwa wananchi, kuwekwa vizuizini na kufanyika kwa mashambulizi mbalimbali. Lengo la hatua hizo lilikuwa ni kuweka masharti na maagizo zaidi kwa nia ya kuvuruga maadhimisho, kuyazuia na kuchochea vita vya kimadhehebu dhidi ya Mashia, Serikali ilianza mwezi wa Muharram kwa kutoa vitisho kwa viongozi wa Husainiyya na majlisi za maombolezo, kisha ikaweka masharti ya kiusalama yasiyo ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuamua namna ya kuonesha alama za maombolezo na kuvaa mavazi meusi, kupanga nyakati za kufanyika kwa majlisi na mawakibu, pamoja na kuwasiliana na makumi ya washairi na wahubiri ili kuwapiga marufuku kushiriki katika shughuli za kidini.
Jumuiya ya Al-Wefaq pia ilieleza kuwa; wahubiri kumi na sita wa Hussein kutoka miongoni mwa wanazuoni wa dini pamoja na washairi watano maarufu walikamatwa wakati wa maadhimisho ya maombolezo. Aidha, idadi nyingine ya wahubiri, washairi na viongozi wa Husainiyya waliitwa na vyombo vya usalama, wakahojiwa na kushikiliwa kwa saa kadhaa katika hatua zilizolenga kuwawekea vikwazo na kuwatisha.
Jumuiya hiyo iliongeza kuwa; maafisa wa utawala wa Aal Khalifa wameyageuza maeneo mbalimbali kuwa viwanja vya mapambano na uvamizi wa mchana na usiku kwa lengo la kuondoa alama za Ashura. Katika operesheni hizo, nguvu na gesi za kuzuia pumzi zilitumika dhidi ya wananchi waliopinga hatua hizo, jambo lililosababisha hali ya taharuki na kuyumbisha usalama wa maadhimisho hayo. Vilevile, washiriki wa majlisi za maombolezo katika mji mkuu wa Manama walifuatiliwa, huku mitaa ya mji huo ikigeuzwa kuwa maeneo ya kuwafukuza, kuwakamata na kuwatisha waombolezaji, hali iliyosababisha kukamatwa zaidi ya wananchi kumi na tano katika siku tofauti.
Jumuiya ya Al-Wefaq iliongeza kuwa; mamlaka ya Bahrain ilipuuza malalamiko ya Husainiyya na majlisi za maombolezo hamsini na tano kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambazo zilikuwa zimetia saini taarifa ya kupinga hatua na maamuzi yaliyohusiana na maadhimisho ya mwezi wa Muharram. Serikali haikutoa maelezo yoyote ya kisheria wala ya kiutawala kuhusu hatua zake, aidha, maafisa wa utawala wa Bahrain waliweka ulinzi mkali katika mji wa Manama ili kuzuia kufanyika kwa ibada ya usiku wa tarehe kumi Muharram, ambayo kila mwaka hufanyika katika mkusanyiko wa pamoja, wakati huo huo, wanazuoni wa dini waliamua kutofanya hafla yao ya kila mwaka kutokana na kuendelea kuzuiliwa kwa wanazuoni wa dini hamsini na sita, wakiwemo wanazuoni wakubwa na walimu wa hawza, licha ya kuwa zaidi ya miongo miwili imepita tangu kuanzishwa kwa utamaduni huo.
Maoni yako